Back to top

Waziri Ndalichako: Kikokotoo kipya kuweka uwiano na usawa wa mafao.

25 June 2022
Share

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amefafanua kuwa kikokotoo kipya kinachotarajiwa kuanza tarehe 1 Julai mwaka huu, 2022, faida yake kubwa ni kuweka uwiano na usawa wa mafao baina ya wastaafu, ambapo watumishi wote wa sekta binafsi na umma watalipwa mafao ya mkupuo wa asilimia 33.

Akiongea wakati wa akichangia mjadala makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2022/2023.Mhe. Ndalichako ameeleza kuwa kikokotoo kipya kinaweka wafanyakazi wote wa Tanzania wa sekta ya binafsi na Umma, ambao wanasimamiwa na sheria za kazi na ajira zinazofanana kutumia viwango sawa vya ukokotozi wa mafao.

“Kikokotoo kipya kitaondoa utofauti kwa wastaafu ambapo baadhi walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 25 wakati wengine walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 50. Kikokotoo hiki kinasaidia kwa sasa mifuko ya pensheni inazungumza lugha moja.”.Prof.Ndalichako.

Mhe. Ndalichako amefafanua kuwa serikali ni sikivu, kutokana na malalamiko ya watumishi na wadau kuhusu Kanuni za mwaka 2018 ambapo watumishi wote walikuwa wanalipwa mafao ya mkupuo kwa asilimia 25.
 
Aidha, ameongeza kuwa makubaliano yaliyofikiwa ndiyo yatakayofanyika kuanzia Julai 1 mwaka huu na kufafanua kuwa kikokotoo kipya kitawasaidia watumishi kwa kuwa aliyechangia milioni 86 na mafao yake ya mkupuo yatapanda kuwa shilingi milioni 71 na ataendelea kulipwa pensheni ya kila mwezi shilingi mil. 1,840,000 mpaka Mwenyezi Mungu atakapo mwita.