Back to top

Waziri Ummy akemea Unyanyapaa kwa wagonjwa wa Corona.

26 March 2020
Share


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu amesema kuwa hadi sasa Tanzania ina wagonjwa wa Corona 13 ambapo 12 wameupata ugonjwa huo nje ya nchi na mmoja ameupata hapa nchini baada ya kukutana na raia kutoka nje ya nchi aliyekuwa na maambukizi, huku akisema mgonjwa wa kwanza wa Corona Isabella ameshapona.

"Kati ya hao wagonjwa 13, Arusha wako 2, Dar es salaam 8, Zanzibar 2 Kagera yuko 1 na kati ya hao ni mmoja tu ambaye hakusafiri nje ya nchi"-Amesema Waziri Ummy. 

Waziri Ummy akizungumza na ITV Digital akiwa jijini Dodoma amesema mpaka kufikia leo Machi 26, 2020 jumla ya watu 273 wamefanyiwa vipimo vya Corona, Tanzania bara (243) na Zanzibar (30), sambamba na kuwafanyia vipimo vya joto wasafiri milioni 1.8 katika vituo 27 vya mipakani ikiwemo viwanja vya ndege na bandarini.

Hata hivyo Waziri Ummy amesema hadi sasa hakuna maambuki ya ndani kwa kuwa kati ya wagonjwa 13 waliopo nchini 12 walisafiri nje ya nchi katika siku 14 zilizopita kabla ya kuthibitika kuugua.

Aidha ameelezea hali ya Isabella ambaye alikuwa mgonjwa wa kwanza kukutwa na maambukizi ya virusi vya Corona ni nzuri na anatakiwa kurudi kwenye jamii na kupokewa bila kunyooshewa kidole na wala kudhalilishwa, na sasa kama serikali inaanza kutoa elimu kwa jamii ya kukataa unyanyapaa kwa waliokuwa wameambukizwa virusi vya COVID 19. 

"Mgonjwa wetu wa kwanza amepona COVID 19, tumepima sampuli mara tatu na zote zimeonyesha negative,tumeanza utaratibu wa kumruhusu kurudi nyumbani"-Waziri Ummy Mwalimu.