Back to top

Wenye viwanda vya mbao waruhusiwa kuendelee na mashine za zamani.

19 February 2019
Share

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameuigiza Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania  (TFS) kuwaruhusu wenye viwanda vya mbao kuendelee kutumia mashine za zamani za kuchakata mbao huku wakiendelea kujipanga kununua mashine za kisasa  kulingana na mabadiliko ya teknolojia.

Hatua hiyo inakuja kufuatia zuio la wamiliki wa viwanda hivyo  kutumia mashine za zamani za kuchakata magogo ambazo zimekuwa zikizalisha taka nyingi na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mbao.

Akizungumza Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanda vya mbao kwa mikoa ya Kaskazini, Ibrahimu Shoo amelalamikia zuio hilo  huku akimuomba Naibu Waziri huyo awape muda wa kutosha kwa ajili ya kujipanga kununua mashine kisasa.

Kufuatia malalamiko hayo, Naibu Waziri huyo ameielekeza TFS iendelee kutoa  leseni na mgao wa vitalu vya miti kwa wamiliki wa viwanda wenye mashine za zamani ili kuweza  kutoa fursa kwao kuweza kujipanga kununua mashine ambazo zinazalisha taka chache wakati wa uchakataji wa mbao

Hata hivyo, Mhe. Kanyasu  amewaeleza Wadau hao kuwa maamuzi ya  kubadili teknolojia ya kutumia mashine mpya zitakazosaidia kupunguza  hasara ya upotevu mkubwa wa mbao bado yapo pale pale.

Aidha, Amesema maamuzi ya kuwataka wamiliki wa viwanda vya mbao kutumia mashine hizo mpya linakwenda sambamba na zuio lililokuwa limetolewa siku za nyuma za kutumia misumeno ya Dingdong ambayo nayo ilikuwa ikisababisha upotevu mkubwa wa mbao.

Pia, Ameagiza TFS itoe  mikataba ya miaka miwili ya ugawaji wa vitalu vya miti kwa Wamiliki wa viwanda vya mbao hali itakayowasaidia kutoa uhakika kwa wamiliki wa viwanda hao kuweza kukopesheka katika mabenki nchini.