Back to top

Wizara ya Afya na WHO zasambaza vifaa mipakani kudhibiti Ebola.

13 September 2018
Share

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na shirika la afya duniani WHO imesambaza vifaa muhimu katika maeneo yote ya mpakani ikiwa ni jitihada za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ikiwa utaingia nchini kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambako umelipuka kwa mara ya kumi mwezi uliopita.

Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt.Lenard Subi amesema wamepokea msaada wa shilingi bilioni tano kwa ajili ya kujikinga na kuwa tayari kutoa huduma kwa wagonjwa ambapo tayari watumishi afya na watumishi wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyombo vya dola hasa walio mipakani wamefundishwa namna ya kufanya uchunguzi wa awali, kumtambua mgonjwa na masuala mengine yatayohakikisha nchi inakuwa salama. 

Kwa upande wake Naibu Afisa Uhamiaji mkoa wa Kigoma Augustino Matheo amesema idara hiyo imejizatiti kudhibiti raia toka nchi jirani wanaoingia nchini na kuomba wananchi kutoa ushirikiano huku nahodha wa meli ya MV.Liemba inayofanya safari zake kutoka kigoma kwenda Zambia Titus Mnyanyi akieleza kuwa hivi sasa wanafanya uchunguzi na kutoa elimu kabla ya meli kuondoka kupitia ziwa Tanganyika. 

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotokea mwezi uliopita nchini DRC ni wa kumi, huku katika milipuko yote ikisababisha watu tisini kufa na hivi sasa wagonjwa zaidi ya mia moja 30 wakiendelea kupatiwa matibabu katika jimbo la Kivu Kaskazini.