
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa, amesema wizara yake iko mbioni kutoa elimu nyepesi kwa wananchi kuhusu hatua mbalimbali za umiliki ardhi na jinsi ardhi inavyoweza kuhamishwa kutoka mmiliki mmoja kwenda kwa mwingine.
Silaa amesema pamoja na wizara yake kuwa na jukumu la kuisimamia ardhi ipo haja kutoa elimu nyepesi kwa watanzania kwenye eneo la ardhi kuanzia inapotwaliwa, kupangwa, kupimwa na kumilikishwa hususan inapohama kutoka mmiliki mmoja kwenda mwingine.
Waziri Silaa amebainisha kuwa anayenunua ardhi kwa mtu anao wajibu wa kujua ama kufahamu aliyemuuzia ameipataje ardhi ambapo amesema maeneo mengine na mauzo hayo yanashuhudiwa na viongozi wakiwemo wenyeviti wa vitongoji.
Amesema hayo wakati wa akizindua Clinic ya Ardhi kwa wilaya ya Bagamoyo inayoendelea eneo la Mapinga mkoa wa Pwani.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, pamoja na wamiliki wa ardhi wa kulinda maeneo yao wanayomiliki lakini wizara yake haitaacha maeneo kama Mapinga Bagamoyo kuwa kichaka cha mtu yeyote mwenye uwezo kufanya anachotaka anafanya.
Amewataka wananchi kuheshimu sheria zinazotungwa na Bunge sambamba na kujifunza kusimamia haki zao.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okashi alieleza kuwa, Clinic ya Ardhi waliyoianzisaha itakuwa na jukumu la kusikiliza kero za wananchi katika masuala ya mbalimbali ya ardhi huku akibainisha kuwa, itaendelea katika kata zote za wilaya ya Bagamoyo.
Uzinduzi wa Clinic ya Ardhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani unafuatia uzinduzi wa Clinic kama hizo kwenye wilaya ya Kigamboni na Temeke ambapo lengu kubwa ni kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za sekta ya ardhi.
