
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imeanza maboresho katika maeneo ya vyuo vyake vya Ardhi vya Morogoro (ARIMO) na Tabora (ARITA)
Hayo yamebainishwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geofrey Pinda, amesema wizara yake imeanza kufanya Mapitio ya Sera ya Wizara aliyoieleza kuwa ni ya siku nyingi na iliyojaa mapungufu ambapo ameweka wazi kuwa, sera pendekezwa tayari imekamilika na kuwasilishwa kwa wadau pamoja na Baraza la Mawaziri.
Mhe.Pinda amesema Sera hiyo imetoa msukumo mpya wa vyuo vya kati vya Morogoro na Tabora pamoja na Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo ya Taarifa za Kijiografia kilichoanzishwa Dodoma na kuzinduliwa hivi karibuni na Naibu Waziri Mkuu Mhe. Dkt.Doto Biteko kuwa na sheria itakayosimamia uendeshaji wa vyuo hivyo.



Amemshukuru Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuijali wizara ya ardhi ambapo amebainisha kuwa, mabadiliko yote yanayoendelea katika wizara hiyo ameridhia kuendelea nayo sambamba na kukubali kuidhinisha miradi mikubwa ya kimkakati yenye fedha nyingi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda amesema, chuo cha ARIMO kina changamoto kadhaa zinazoendelea kushughulikiwa na kubainisha kuwa kati ya changamoto hizo baadhi zinahitaji msukumo wa wizara.
Ametoa mfano wa changamoto zinazohitaji msukumo wa wizara kuwa, ni suala la vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi. Amesema, mafunzo ya chuo hicho yanahitaji umahiri wa kutenda na siyo kusimulia hivyo ni muhimu kwa chuo kuwa na vifaa vya kutosha vya kujifunza umahiri huo wanaoenda kuufanya wanafunzi katika soko.
Ameitaja changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya chuo inayoendelea kushughulikiea na chuo ambapo hata hivyo amesema chuo hicho cha ARIMO tayari kinao mpango kabambe alioueleza kuwa ana imani utakuwa muaroabini wa changamoto hiyo.
