Back to top

Wizara ya fedha kurejesha mahusiano mazuri na wafanyabiashara.

06 April 2021
Share

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt.Mwigulu Nchemba amewahakikishia wafanyabiashara hapa nchini kuwa Wizara yake itahakikisha inarejesha taswira na uhusiano mzuri nao katika masuala ya kodi ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kusisimua uchumi wa nchi.

Waziri Nchemba ametoa ahadi hiyo Ikulu Jijini Dar es Salaam alipozungumza na vyombo vya habari, baada ya tukio la kuapishwa kwa Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu pamoja na viongozi wa Taasisi, tukio lililofanywa na Rais wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan.

Amesema Serikali itatengeneza vyanzo vipya vya makusanyo ili mzigo wa kodi usibebwe na wachache kwa sababu kadri mzigo unavyobebwa na wengi ndivyo nafuu inavyopatikana, hatua itakayowafanya wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari.

Kuhusu udhibiti wa matumizi wa Fedha za Umma, Dkt.Nchemba amesema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itatumia mifumo ya fedha iliyobuniwa kudhibiti matumizi ya Serikali na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili iwe michache.