Back to top

ZIARA YA RAIS SAMIA KOREA, MIKATABA 7 KUSAINIWA

29 May 2024
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuanza ziara ya siku sita nchini Korea Kusini kuanzia Mei 30, 2024, kwa mwaliko rasmi wa kiongozi mkuu wa Taifa hilo.
.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe.January Makamba, wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za Wizara hiyo zilizopo Jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa katika ziara hiyo, Serikali ya Tanzania itaingia mikataba saba ukiwemo wa msaada na mkopo nafuu wa Dola za Marekani bilioni 2.5 kutoka katika Serikali ya Korea Kusini.
.
Waziri Makamba ametaja mikataba mingine itakayosainiwa ni pamoja na ushirikiano katika maendeleo ya uchumi wa buluu, kutambua vyeti vya mabaharia, tamko la pamoja la uanzishwaji wa majadiliano na mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi.
.
Mingine ni hati ya makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi na Miamba na Madini ya Korea, ushirikiano utakaojikita katika utafiti, uchoraji ramani, rasilimali na shughuli za maabara.
.
Mbali na hilo, Waziri Makamba amesema kutakuwa na hati ya makubaliano kati ya Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Viwanda na Biashara ya Korea kuhusu ushirikiano wa kuchambua na kufanya utafiti wa madini mkakati.
.
Halikadhalika kutasainiwa mkataba wa makubaliano kati ya Shirika la Taifa la Madini (Stamico) na Shirika la Ukarabati wa Migodina Rasilimali za Madini la Korea.
.
Waziri Makamba amesema ziara hiyo, pia  itaanzisha ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Korea cha Usafiri wa Anga na Tanzania ili kuboresha soko la usafiri wa anga na uendeshwaji wa biashara ya sekta hiyo.Pia uendeshaji na uratibu wa viwanja vya ndege, utalaamu,utafiti na huduma.
.
Mbali na hilo, Waziri Makamba amesema kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwenye menejimenti ya usafiri wa anga nchi ikiwemo miundombinu ya ukabarati na ujenzi wa  viwanja na udhibiti na ufufuaji wa usafiri wa anga.
.
Chuo Kikuu cha Masuala ya Anga cha Korea kitamtunuku Rais Samia shahada ya heshima ya udaktari katika menejimenti ya usafiri wa anga, Rais Samia atashiriki pia mkutano wa wakuu wa nchi kati ya Korea na Afrika utakaoanza Juni 3 hadi 4 na mkuu huyo wa nchi atapata nafasi ya kuhutubia na kuzungumza katika jopo moja kati ya manne yatakayokuwapo.