Back to top

Zoezi la uokoaji wachimbaji wawili wa madini laingia siku ya 6.

06 October 2019
Share


Timu ya uokoaji kutoka kundi la wachimbaji wadogo katika mgodi wa Imalanguzu Mkoani Geita imelazimika kusitisha zoezi la kuwaokoa  wachimbaji wawili waliofukiwa na kifusi kwa saa nane kutokana na magogo ya miti yaliyopo ndani ya mgodi huo kuziba njia na kuhatarisha usalama wao.

Wameiomba Serikali kuongeza vifaa na watalamu wa uokoaji ili kuendelea na zoezi hilo ambalo limeingia siku ya sita sasa.

Kikosi hicho cha uokoaji kinachoshirikiana na kikosi cha Zima Moto na Uokoaji pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa siku sita sasa wamesema mazingira ya mgodi huo yamekuwa hatarishi kutokana na magogo yaliyotumika kujengea mgodi huo kuoza na kushindwa kuhimili maporomoko ya udongo.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Geita, Bwana Zabloni Mhuma amesema baada ya zoezi hilo kukwama,  wameamua kutumia njia mbadala ya kuchimba nje ya mgodi ili kukwepa mgodi huo kuporomoka.