Back to top

RAIS SAMIA AWATAKA WADAU WA SHERIA KUTENDA HAKI

01 February 2024
Share

Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na wadau wa usuluhishi kubainisha maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ikiwemo kutunga sera ya usuluhishi.

Rais Samia amesema ni wakati muafaka wa kujielekeza kufanya utatuzi kwa njia ya usuluhishi bila kufungwa na masharti ya kiufundi yanayokwamisha kutenda haki.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akihutubia katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kwenye viwanja vya Chinangali Dodoma.

Rais Samia pia ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau kutekeleza kikamilifu utoaji wa msaada wa kisheria kwa kuzingatia Ibara ya 107A ya Katiba inayowataka kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali zao za kijamii au kiuchumi.

Rais Samia amesisitiza kuwa ni vyema Mahakama ikatoa kipaumbele cha kuharakishwa usikilizwaji wa kesi za kibiashara katika masuala ya kisheria pindi inapotokea migogoro ili kuvutia mitaji na uwekezaji na kufungua fursa za biashara.