
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeshiriki katika maonyesho ya 52 ya Kimataifa ya Uwindaji wa Kitalii yanayoratibiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Marekani inayojulikana kama 'Safari Club International SCI'.
Kabla ya kushiriki katika maonyesho hayo, wajumbe kutoka Tanzania walipata nafasi ya kukutana na Balozi wa Tanzania Nchini Marekani Dk.Elsie Kanza, pamoja na kujitambulisha kwa Balozi, wajumbe hao walijadili mambo mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kushirikisha wadau wa ndani na nje katika kutoa elimu kuhusu umuhimu wa uwindaji wa kitalii katika kuimarisha uhifadhi, kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Aidha,Balozi alihaidi kuunganisha tasnia ya uwindaji wa kitalii ya Tanzania na Mamlaka za Serikali ya Marekani.






Ujumbe wa TAWA uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (mst) Hamis Semfuko, akiambatana na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi - Huduma za Utalii na Biashara Fredrick Ligate na Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Matumizi Endelevu ya Wanyamapori - Arusha Lucy Lyimo.
Tanzania ilipata nafasi ya kipekee ya kukutana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Congress inayohusika na Maliasili (House Committee on Natural Resources Chairman) Bruce Westerman ambapo mambo mbalimbali yanayohusu ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani yalijadiliwa ikiwemo masuala ya uwekezaji katika sekta ya utalii na mchango wa tasnia ya uwindaji wa kitalii kiuchumi, kiikolojia na kijamii.
