
Watu 9 wamefikishwa katika mahakama ya Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza, wakituhumiwa kufanya mauaji ya aliyekuwa mlinzi wa duka, aliyefahamika kwa jina la Yumeni Elias Dotto (54), Mkazi wa Nyashishi, Jijini humo.
.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe.Juma Mpuya, Mwendesha Mashtaka wa Jeshi la Polisi, George Ngemela amesema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo mnamo Januari 15, 2024, katika Mtaa wa Mwananchi Jijini Mwanza, baada ya kumvamia Yumeni Elias Dotto, kisha kumkata na kitu chenye ncha kali kichwani, hali iliyosababisha kifo cha mlinzi huyo.
.
Watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, huku Mwendesha Mashtaka wa Jeshi la Polisi, akiomba shauri hilo lipangiwe tarehe nyingine kwa ajili kusomwa tena, kwani Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi.
.
Watuhumiwa hao ni Julius Joseph mkazi wa Igoma-Mwanza, Paul John mkazi wa Mwananchi-Mwanza, Leonidas Juma Bukwimba maarufu kama Wa Dar mkazi wa Buhongwa-Mwanza, Abdalah Hasan maarufu kama Dulla mkazi wa Nundu-Mwanza, Edward Boniface mkazi wa Mahina-Mwanza, Mussa Robert mkazi wa Ilemela Kanisani-Mwanza, Steven Emanuel mkazi wa Nyakato-Mwanza, George Mang'erakoloso mkazi wa Nyegezi-Mwanza na Charles Chaca mkazi wa Mahina-Mwanza.
.
Watuhumiwa ambao walikamatwa kwa nyakati tofauti Jijini humo, wote wamerudishwa Mahabusu katika gereza kuu la Butimba hadi Februari 20, 2024, shauri hilo litakaposomwa tena mahakamani hapo baada ya upelelezi kukamilika tena.
