Back to top

RAIS MWINYI ATOA AGIZO KUANZA KAZI MAHAKAMA YA RUSHWA 

07 February 2024
Share

Rais wa Zanzibar ambaye pia Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi, ameagiza taasisi zinazohusika na sheria kukamilisha mchakato wa utungaji wa sheria, ili kuanza kazi kwa Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi, kwa mwaka huu.

Rais Dk.Mwinyi amesema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya siku ya Sheria Zanzibar,katika viwanja vya Mahakama kuu Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Rais Dk.Mwinyi amesema ustawi bora wa wananchi utategemea kuwepo kwa misingi imara ya kuheshimu haki za binadamu, utawala bora, uhuru wa Mahkama pamoja na sheria madhubuti zinazoilinda jamii dhidi ya aina zote za unyanyasaji. 

Aidha ameipongeza Mahakama ya Zanzibar kwa kuanza  mchakato wa kuboresha mfumo wa kieletroniki wa usikilizaji wa mashauri kwa msaada wa kitalaamu kutoka Mahakama ya Tanzania.

Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi amezindua mpango mkakati wa miaka mitano wa Mahkama (2024-2029) na kukabidhiwa ripoti ya utendaji kazi wa Mahkama ya mwaka 2023.