
Mahakama kuu Tanzania Kanda ya Iringa imemwachia huru Maria Ngoda maarufu "Mjane wa Nyama ya Swala", Aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 22 jela kwa kosa la kukutwa na vipande kumi na mbili vya nyama iliyodaiwa kuwa ni ya swala.
.
Akisoma hukumu ya shauri la rufaa namba 84101la mwaka 2023 Maria Ngoda dhidi ya Jamuhuri, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Iringa Mheshimiwa Ilvin Mugeta amesema mahakama imejiridhisha pasipo na shaka kuwa adhabu aliyopewa mrufani Bi. Maria Ngoda haikuzingatia misingi ya kisheria ikiwemo kujiridhisha pasipo na shaka kuwa kidhibiti anachodaiwa kukutwa nacho mrufani Maria Ngoda, kilikuwa ni mali yake.
.
Ameongeza kuwa katika kipengele hicho mashahidi wa upande wa Jamhuri akiwemo askari wa Jeshi la polisi aliyemkamata Mrufani Maria Ngoda na Mwenyekiti wa Mtaa wa Isakalilo walishindwa kuthibitisha pasipo shaka umiliki wa vipande hivyo kumi na mbili vya nyama ya swala kwa mrufani Maria Ngoda.
.
Katika rufaa yake kupinga hukumu ya miaka 22 jela aliyohukumiwa novemba 03, 2023 katika mahakama yaWilaya ya Iringa mrufani Maria Ngoda aliwskilishwa na mawakili sita kutoka chama cha wanasheria Tanganyika TLS mkoa wa Iringa huku upande wa jamhuri ukiwakilishwa na mawakili watatu ambapo katika moja ya hoja zilizobishaniwa mahakamani hapo ni ushahidi wa kidhibiti alichodaiwa kukutwa nacho mrufani Maria Ngoda huko Isakalilo ambacho ni vipande kumi na mbili vya nyama ya swala na namna kidhibiti hicho kilivyotunzwa.
.
Mheshimiwa Jaji Elvin Mgeta amesema upande wa Jamuhuri ulishindwa kuthibitisha pasipo shaka kuwa vipande hivyo vya nyama ilikuwa ni nyama ya swala huku pia jeshi la polisi likishindwa kufuata taratibu za kisheria kuharibu kidhibiti hicho ambapo Jaji mheshimiwa Ilvin Mgeta amesema katika hukumu hiyo kuwa mahakama iliyomuhukumu mrufani katika shauri mama la kukutwa na vipande hivyo vya nyama ilishindwa kuzingatia utetezi wa mrufani Maria Ngoda ambaye alikamatwa kwa kukutwa eneo la tukio na siyo kukamatwa akiwa na ndoo iliyokuwa na vipande hivyo vya nyama ya swala.
