Back to top

MUHIMBILI WAFANYA UPASUAJI KUOTESHA NYWELE KWENYE KIPARA

18 February 2024
Share

Watalaam wa upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kushirikiana na wenzao kutoka nchini Marekani, wamefanikiwa kufanya upasuaji wakuotesha nywele kwenye kipara, kwa watu nane akiwemo mtoto ambaye alizaliwa kichwa chake kikiwa na vinundu vidogo vidogo mithili ya visunzua (skin tag), ambavyo baada ya kuondolewa vilifanya sehemu kubwa ya kichwa chake kuwa na kipara.
.
Wataalamu hao wamefanya upasuaji huo kupitia kambi maalum ya siku tano iliyohusisha upasuaji wa urembo na upasuaji wa matibabu (Cosmetic and Reconstructive Surgery), ambao hufanywa kwa wagonjwa waliokuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo waliopata ajali ya kuungua moto na wenye misuli iliyokakamaa kutokana na majeraha.
.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo, kwa niaba ya timu nzima iliyoshiriki, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa MNH, Dkt. Ibrahim Mkoma, amesema mtoto huyo amewekewa puto (tissue expander) kwenye kichwa katika sehemu yenye nywele karibu na kipara ili ngozi ya eneo hilo iweze kuongezeka na kukuza nywele, ambazo baada ya mwezi mmoja zitakuwa zimeota sehemu kubwa na kuruhusu kufanyiwa upasuaji wa kuvuta ngozi hiyo, ikiwa na nywele na kufunika sehemu yenye kipara hivyo kumwezesha mtoto huyo kurudi katika hali yake ya kawaida.