
Zaidi ya abiria 65 wamenusurika kifo baada ya Basi la kampuni ya Best Line walilokuwa wakisafiria kutoka jiji la Mbeya kuelekea mkoani Mwanza kupinduka katika eneo la Shamwengo, kijiji cha Ilongo mkoani Mbeya.
Basi la kampuni ya Best Line linalofanya safari zake kati ya jiji la Mbeya na jiji la Mwanza leo limeondoka kituo kikuu cha mabasi cha jijini Mbeya likiwa na abiria zaidi ya 65 na lilipofika katika mtelemko mkali wa mlima Shamwengo likapata ajali baada ya kupinduka ambapo mashuhuda na abiria waliokuwa ndani ya gari hilo wamesema sababu ya kupinduka kwa gari hilo ni dereva kujaribu kulikwepa lori lililosimama ghafla mbele ya basi hilo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Naibu Kamshina wa jeshi la Polisi, DCP Mohamed Mpinga amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kudai kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori aina ya Fuso ambalo likuwa likilipita gari la mbele yake bila tahadhari na kutaka kugongana uso kwa uso na basi la Best Line na ndipo dereva wa basi akaamua kuepusha ajali ya kugongana uso kwa uso na kuliingiza gari mtaroni.
Jeshi la polisi mkoani Mbeya limehimiza abiria wote wanaotumia usafiri wa magari kufunga mikanda ya usalama kila wawapo safarini kwa madai kuwa kama abiria wa basi la Best Line wasingekuwa wamefunga mikanda ya usalama huwenda ajali hiyo ingesababisha vifo au majeruhi.