Back to top

RAIS SAMIA AWAPANDISHA VYEO MAOFISA WA POLISI.

19 February 2024
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Dk. Samia Suluhu Hassan, amewapandisha vyeo maofisa wa Polisi 155.

Waliopandishwa vyeo ni pamoja na Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi, kuwa Manaibu Kamishna wa Polisi ambao wapo 27, na Makamishna Wasaidizi wa Polisi kuwa Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Polisi wapo 128 ambao wamekula kiapo cha Utii kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi na Kiapo cha Maadili ya Viongozi wa Umma.

Akitoa nasaha zake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura amesema kuwa, kupandishwa vyeo kwa maofisa hao kutaongeza chachu ya utendaji kazi, kutenda haki, uadilifu na nidhamu pia wananchi wategemee mabadiliko makubwa ya kiutendaji.

Naye Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu CP Susan Kaganda amesema miongoni mwa waliopandishwa vyeo pia wapo maofisa nane wa kike ambao wamepanda vyeo na kuwa Manaibu Kamishna wa Polisi.

Akizungumza kwa niaba ya waliopandishwa vyeo Msemaji wa Jeshi la Polisi Naibu Kamishna wa Polisi David Misime amesema kupanda kwao vyeo kutaongeza morali na utimamu zaidi wa akili katika kutekeleza majukumu ya kazi za Polisi.