Back to top

SILAA AKABIDHI MAGARI 16 KUTEKELEZA MRADI WA LTIP

19 February 2024
Share

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Jerry Silaa, amekabidhi magari 16 yenye thamani zaidi ya Shilingi bilioni 2 ambayo yatatumika kwenye Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa hapa nchini.

Waziri Silaa amesema hayo katika Mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma, wakati akikabidhi magari hayo kwa Katibu Mkuu ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga, na kusisitiza kuwa magari hayo yatumike kwa kazi ya mradi, wale wote watakaokabidhiwa magari hayo wayatumie vizuri, wayatunze. 

Pia amesema anataka kuyaona magari hayo yakifanyakazi na kuongeza kasi ya utekelezaji wa uboreshaji wa milki, kazi ya matumizi bora ya ardhi vijijini na kazi ya urasimishaji katika Halmashauri mijini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Anthony Sanga, amesema Mradi huo unaotekelezwa nchini chini ya Wizara ya Adhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi unagharimu zaidi shilingi bilioni 346 ambazo ni sawa na dola za Kimarekani milioni 150.

Naye Mratibu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) Bw. Joseph Shewiyo amesema mradi huo unajukumu la kusimamia usalama wa milki za ardhi mijini na vijijini ambapo amewahamasisha wanandoa wawe na umiliki wa ardhi wa pamoja.

Mradi huo ni wa miaka mitano kuanzia 2022 hadi 2027 unatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.