
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeanza kusoma hukumu ya kesi ya mauaji inayomkabili Miriam Steven Mrita, mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa madini mkoani Arusha, bilionea Erasto Msuya.
Katika viunga vya mahakama ya kuu hali ni tulivu na Jaji anayesoma hukumu hiyo ni Mh. Edwin Kalokola ambapo ndugu wa pande zote wanaonekana kuwa watulivu wakifuatilia shauri hilo kwa umakini mkubwa.
Miriam pamoja na mshitakiwa mwenzake, Revocatus Everist Muyella, maarufu kama Ray, wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kukusudia, wanadaiwa kumuua kwa kumchinja, Aneth Elisaria Msuya ambaye ni wifi yake Miriam.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 103 ya mwaka 2018, Miriam na mwenzake Muyella wanadaiwa kutenda kosa hilo la mauaji ya kukusudia Mei 26, 2016 huko nyumbani kwa Aneth, Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Aneth alikuwa mdogo wa bilionea Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwa kutumia bunduki ya kivita aina ya SMG eneo la Mijohoroni, Barabara Kuu ya Moshi-Arusha wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, Agosti 7, 2013.
