Back to top

MLOGANZILA YAZALISHA BIL. 8, KUTOKANA NA TIBA UREMBO

24 February 2024
Share

Naibu Waziri wa Afya, Mhe.Dkt.Godwin Mollel, amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, imezalisha Shilingi Bilioni 8, kwa kufanya tiba urembo.
.
Dkt.Mollel ameyasema hayo katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, kwenye Hospitali hiyo ambapo amebainisha kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya hasa kwenye miundombinu, teknolojia ya afya pamoja na wataalamu, kwani sasa kuna wataalamu wa kutosha kwenye masuala mbalimbali ya utoaji huduma za afya hapa nchini.
.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile, amesema wameridhishwa na hali ya utoaji huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, kuanzia kwa wafanyakazi, vifaa bora na vya kisasa pamoja  mazingira ambayo amesisitiza kuwa yanaridhisha na wagonjwa wanahudumiwa vizuri.
.
Pia, Dkt.Ndungulile ameipongeza Serikali kutokana na uwekezaji inaoendelea kuufanya katika sekta ya Afya, kwani kutokana na uwekezaji huo hivi sasa 90% ya wagonjwa waliokuwa wanaenda nje ya nchi kutibiwa wanatibiwa hapa nchini na tumeanza kupokea wagonjwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.
.


“Niipongeze Serikali kwa kuboresha huduma za afya nchini kwani hivi sasa asilimia 90 ya wagonjwa ambao walikuwa wanakwenda nje ya nchi kutibiwa wanatibiwa hapa nchini na tumeanza kupata wageni kutoka nje ya nchi kuja kupata huduma nchini”. Alieleza Dkt. Ndungulile.


.
Aidha, ameitaka Serikali kupanua wigo wa utoaji huduma katika hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwani hospitali hiyo bado ina eneo kubwa ambapo kuna takribani ekari 3800.
.


"Tunahitaji upanuzi wa huduma za magonjwa ya moyo, upanuzi wa huduma za saratani, upanuzi wa huduma za magonjwa mengine ya mifupa na mfumo wa ubongo ili wananchi waweze kupata huduma bora na rahisi kwa wepesi zaidi hapa nchini". Alisema Dkt. Ndugulile.


.
Vile vile  ameongeza kuwa kuna fedha wameambiwa zimepatikana, ujenzi unashindwa kuendelea kwa sababu ya masuala ya umiliki wa ardhi hayajakamilika hivyo kamati hiyo imeitaka Serikali kupitia Wizara ya afya na Wizara ya Elimu kukaa pamoja ili kuweza kufikia muafaka ili uwekezaji uweze kufanyika kwa sababu wananchi wanahitaji huduma bora zaidi na eneo hilo linatosha kwa matumizi yote ya elimu pamoja na huduma za afya.