
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe (Tupindo) mkoani Katavi.
Mhe.Pinada amesema uwekezaji uliofanyika katika hospitali hiyo hasa kuwekwa vifaa vya X-Ray na Utra Sound, utachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa wagonjwa kutoka nje ya Halmashauri hiyo wakiwemo wale wa Sumbawanga Vijijini katika maeneo ya Finga, Mtowiza na Muze.
Mhe. Pinda ametoa shukrani hizo alipotembelea na kukagua shughuli zinazofanyika katika hospitali hiyo iliyopo kitongoji cha Tupindo kata ya Mbede wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.



Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe (Tupindo) Dkt.Rio Ernest hospitali, amesema, hospitali hiyo kwa sasa inavyo vitengo mbalimbali vyenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa na kuvitaja kuwa ni kitengo cha Afya ya kinywa, Macho, Mionzi, Wazazi, Maabara pamoja na Wagonjwa wa nje na ndani.
Hata hivyo, ameeleza kuwa, pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika zipo changamoto kadhaa kama vile uchache wa watumishi jambo alilolieleza kuwa linalopelekea baadhi ya vitengo kutofanya kazi kwa saa 24 na kutolea mfano wa vitengo vya Famasia, Mionzi na Maabara.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni barabara za ndani ya hospitali pamoja na ukosefu mitaro ya kutoa maji ndani ya eneo la hospitali. Pia ukosefu wa uzio unaosababisha usalama kwa wagonjwa, watoa huduma na mali za hospitali.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Mwariko amemueleza Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Pinda kuwa, uwekezaji uliofanyika katika hospitali hiyo kumesababisha kuongezeka kwa mapato ya hospitali.
Hospitali ya Halmashauri ya Mpimbwe (Tupindo), ilianza kutoa huduma mwaka 2020 na kwa sasa hospitali hiyo inaendelea kukua kwa kasi kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.
