
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara Mhandisi Dutu Masele amesema serikali imedhamiria kuinua Uchumi wa Wananchi na pato la Taifa kwa kuufungua mkoa huo kwa ujenzi wa barabara za lami ambazo zitaunganisha uchumi wa Kanda ya Ziwa na Nchi Jirani za Burundi, Uganda na Rwanda kwa kutumia Bandari ya Tanga.
Mhandisi Dutu Masele amesema Amesema miradi mikubwa mitatu kati ya saba ya Kitaifa ya ujenzi wa barabara ambayo tayari serikali kupitia TANROADS ilishasaini, ni mikataba kwa ajili ya ujenzi itapita katika Mkoa wa Manyara.
Mhandisi Dutu Masele amebainisha hayo akiongea na wanahabari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya ujenzi wa Miundombinu.




Ameeleza kuwa miradi hiyo inayotekelezwa kwa kushirikiana na wabia kwa mfumo wa EPC + F inaanzia Handeni mkoani Tanga – Kiteto Manyara – Chemba Dodoma hadi Singida, katika mradi huo Mkoa wa Manyara una jumla ya Kilomita 120, mradi mwingine ni ule unaounganisha Mkoa wa Dodoma – Manyara na Arusha (Arusha – Kibaya – Kongwa) Mkoa wa Manyara una jumla ya Kilomita 333.
Mradi wa tatu amesema ni wa Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiti, Lalago hadi Maswa wa kilomita 389, kati ya hizo kilomita 50 zipo katika Mkoa wa Manyara na ziko kwenye utaratibu wa ujenzi kwa fedha za ndani.
"Tunaipongeza Serikali kwa kuona namna sasa kuufungua Mkoa wa Manyara kwa maana katika miradi yote saba yenye urefu wa kilometa 2,035 itakayotekelezwa nchi nzima kwa utaratibu wa EPC + F; kilomita 515 zipo katika Mkoa wa Manyara"amesema Masele.




