Back to top

Vituo 9 vya afya vyafungiwa mkoani Morogoro.

29 March 2018
Share

Serikali kupitia Bodi ya ushauri wa hospitali binafsi iliyo chini ya Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,jinsia,wazee na watoto imevifungia vituo tisa vya afya mkoani Morogoro baada ya kubainika kufanya kazi bila kukidhi vigezo mbalimbali ikiwemo kukosa usajili na kutibu wagonjwa bila kuwa na sifa stahili.

Kufungwa kwa vituo hivyo vya afya kumefanywa wakati wa kaguzi za kushtukiza  katika maeneo mbalimbali ya wilaya za mkoa wa Morogoro ambapo  mapungufu yaliyoibuliwa ni pamoja na vituo vingi kushindwa kutimiza matakwa ya sheria na kufanya kazi bila kuwa na usajili ambapo faini za papo kwa papo zimetozwa sambamba na kufungiwa kwa baadhi ya wamiliki wa vituo wakisubiri hatua zaidi ikiwemo kufikishwa mahakamani.

Mjumbe wa Sekretarieti ya bodi hiyo John Kasambula amesema baadhi ya changamoto nyingi zimechangiwa na usimamizi mdogo kutoka ngazi ya mkoa na kubainisha adhabu zaidi zitachukuliwa kwa watakaokuwa wamefungiwa na kukaidi kusitisha huduma ambapo baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo pamoja na kudai kutotambua baadhi ya sheria hizo wameeleza kupokea vyema kaguzi hizo na kuomba zoezi hilo kufanywa hata ktk vituo vya serikali.

Zoezi hilo limetajwa kuwa ni endelevu huku wanao endesha vituo bila kufuata taratibu wakitakiwa kusitisha mara moja kutoa huduma.