Back to top

TANROADS WAPEWA SIKU 4 KUKAGUA  MADARAJA NA BARABARA NCHI NZIMA

05 March 2024
Share

Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) nchi nzima wamepewa siku nne za kufanya tathmini na ukaguzi wa madaraja, makalvati na barabara kuu zote ambazo zimekuwa zikifanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kuwasilisha taarifa hizo kwa wakuu wa Mikoa ili serikali iweze kuchukua hatua ya haraka.

Agizo hilo limetolewa mkoani Lindi na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa,  kufuatia taarifa ya Mamlaka ya hali ya hewa, kuhusu maoteo ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, na kuathiri miundombinu ya barabara, madaraja na makalvati kwa baadhi ya maeneo.

“Nielekeze hadi kufika Machi 9 Mwaka huu kila Meneja wa Mkoa wa TANROADS na timu yake wakabidhi taarifa ya hali ya barabara na maeneo ya hatari yanayoweza kujitokeza katika madaraja na makalvati ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka”, amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameiomba Wizara ya Fedha kuendelea kupeleka fedha za dharura katika mikoa yote ili Mameneja wa TANROADS waweze kuendelea kuchukua hatua pale ambapo changamoto za Mvua za El - Nino na mawasiliano ya barabara yanapokatika.

Aidha, amewasihi wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika maeneo yao kama walivyotangaziwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa pindi wanapoona maji mengi yanakatiza juu ya barabara na madaraja ili kulinda usalama wao na vyombo wanavyovitumia.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, ameomba fedha za dharura za matengenezo ya barabara kufika kwa haraka ili ziweze kunusuru barabara zilizoathiriwa na mvua na zile zilizofunga hasa kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale ambao wamekuwa kisiwani hawawezi kutoka wala kuingia.