Back to top

PINDA ATULIZA MGOGORO WA MASHAMBA BABATI

05 March 2024
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Geophrey Pinda, amewatuliza wananchi wa Vijiji vya Kimara na Kiru Dick vilivyopo Halmashauri ya Babati Mkoa wa Manyara, kutokana na mgogoro baina yao na wawekezaji wa mashamba, kufuatia kuingia kwenye mgogoro na wamiliki wa mashamba ya Miombo Estate na Hamir Estate yaliyopo Bonde la Kivu katika halmashauri hiyo.

Mhe.Pinda amezungumza na Wananchi wa Vijiji vya Kimara na Kiru Dick, Wilayani Babati akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo na kuwataka kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kushughulikia mgogoro huo.

Uamuzi huo ni utekelezaji wa agizo la Katibu Mwenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda ambaye katika ziara yake mkoani Manyara alipokea malalamiko kuhusu mgogoro huo na kumuelekeza Pinda kwenda kutafuta suluhu.

Pinda amewakumbusha wananchi wa Vijii vilivyoingia kwenye mgogoro kuwa, wasisahau kwamba uwepo wa wawekezaji kwenye maeneo hayo bado ni halali hivyo wakati serikali ikienda kuweka mambo sawa basi waepuke ushabiki.

Kwa mujibu wa Mhe, Pinda, ujio wake katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa mashamba wilayani Babati ni kusimamisha yale masuala ya kesi kwa zile pande zinazopingana ili zikae meza moja na kumaliza mgogoro kwa lengo la wananchi kuishi kwa amani.

Awali wananchi wa vijiji hivyo walimueleza Mhe, Pinda kuwa, wakati wa kutafuta suluhu ya mgogoro huo ahakikishe makubaliano makubwa ni makazi ya watu kutoguswa sambamba na wao kutambuliwa kwa kuwa wamezaliwa na mababu zao waliokuwa wakiishi maeneo hayo.

Aidha, wamemshukuru Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Pinda kwa kwenda katika vijiji hivyo kutafuta suluhu ya mgogoro huo ambapo wametaka mgogoro huo kumalizwa viziuri ili wananchi waishi vizuri na wawekezaji.

Kwa upande wao wawekezaji wa mashamba ya Miombo na Hamir Estate wamemueleza Mhe, Pinda kuwa hawana nia mbaya na wananchi wa vijiji vinavyowazunguka na kueleza kuwa, hata uamuzi wao wa kuachia sehemu ya maeneo ya mashamba yao wanayomiliki ni kutaka kuishi kwa amani na kuepuka ugomvi na wananchi.