
Wanawake wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kutoka Vituo vya Makao Makuu na Bandari ya Dar es Salaam leo, wameanza Wiki ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, kwa kutoa misaada yenye thamani ya Shilingi Milioni 60 kwa Kituo cha kulea watoto yatima cha Jeshi la Wokovu, Kurasini na Hospitali ya Ocean Road Jijini Dar Es Salaam.
Kabla ya kushiriki matendo ya huruma katika Taasisi hizo, Wanawake hao walishiriki katika zoezi la uchunguzi wa Saratani ya matiti na mlango wa kizazi katika Kituo cha Afya cha TPA linaloratibiwa na Kituo hicho pamoja na Chama cha Madaktari wanawake Tanzania ( MEWATA)
Msaada huo unajumuisha Mahitaji mbali mbali kwa watoto yatima na vifaa tiba.
Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa Mwaka huu 2024 inasema "Wekeza kwa Wanawake Kurahisisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii".
