
Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Nchini (TBS) litajenga vituo maalumu vya ukaguzi wa magari maeneo yote ya mipakani, ambapo itafungwa mitambo ya kisasa kwa ajili ya ukaguzi huo.
Hayo yamesemwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, DCP Ramadhan Ng’anzi, wakati alipofika katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua eneo ambalo kituo hicho kitajengwa kwa mkoa wa Arusha.
Kamanda Ng’anzi amebainisha kuwa vituo hivyo vitatumika kukagua magari yote, ambayo yanaingia nchini toka nchi jirani, kwa ajili ya kukagua ubora wa magari hayo, ambapo yale mabovu hayataruhusiwa kuingia hadi yatakapotengenezwa.
Aidha amewataka wamiliki wa Vyombo vya moto kuhakikisha wanatimiza wajibu wa kisheria wa kukagua vyombo vyao kama inavyoelekezwa katika sheria kwani Jeshi la Polisi halitakuwa na muhali kwa wale watakaoshindwa kutii sheria bila shuruti.
Kwa upande wake Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini Mhandisi Joseph Mwaipaja amesema ameridhishwa na eneo hilo mara baada ya ukaguzi, hivyo Shirika hilo litaleta mitambo hiyo haraka iwekenavyo katika eneo hilo kwa ajili ya kufungwa ili kudhibiti ajali za barabani.
