
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wabobezi kutoka nchini Sudan, imefanya upasuaji rekebishi wa macho ambao unahusisha watu wenye uvimbe nje ya jicho, makengeza kwa watu wazima, majeraha yatokanayo na ajali au makovu ya muda mrefu ya macho, wanaotoka machozi kwa muda mrefu kutokana na kuziba kwa njia za machozi.
Upasuaji huo unafanyika katika kambi maalumu iliyoshirikisha madaktari wazawa kutoka Muhimbili Upanga, Hospitali ya Benjamini Mkapa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi, Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mtwara Ligula, Hospitali ya Kanda Mbeya na St. Benedict Lindi.
Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Macho wa Muhimbili Mloganzila, Catherine Makunja kabla ya kuanza kwa upasuaji huo, jana Machi 11, 2024 jopo la wataalamu liliwaona na kuwafanyia uchunguzi wa awali wagonjwa wenye matatizo hayo ambao wamejitokeza.
Dkt. Makunja amesema kufuatia kuanza kwa kambi hiyo, leo wamefanyia upasuaji wa macho wagonjwa wenye changamoto ya kufunga kwa vifuniko vya macho na zoezi hilo limeenda vizuri bila changamoto zozote na baadhi yao wameruhusiwa kurudi nyumbani .
