
Ujenzi wa Daraja la Kigongo - Busisi, maarufu kama daraja la JPM, linalojengwa kuunganisha Barabara Kuu ya Usagara - Sengerema - Geita, katika Ziwa Victoria umefika asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2024.
Taarifa hiyo imetolewa katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Kakoso ilipoambatana na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kukagua maendeleo ya mradi huo mkoani Mwanza.

Kakoso ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuimarisha mifumo ya ulinzi na usalama katika daraja hilo ambalo linatokana na kodi za wanachi ili liweze kudumu kwa muda wa miaka 100.




Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema mpaka sasa jumla ya Shilingi Bilioni 441.3 zimetolewa kwa ajili ya kumlipa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo.
Awali akitoa taarifa ya mradi, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Doroth Mtenga ameeleza kuwa mradi huo unatumika kama darasa la mafunzo kwa wanafunzi na wataalamu wetu wa ndani kupata uzoefu wa kusimamia na kujenga madaraja mengine kama hayo hapa nchini.
