Back to top

LAAC YATOA MIEZI 3 KITUO CHA AFYA BULELA KIKAMILIKE

20 March 2024
Share

Halmashauri ya Mji wa Geita imepewa miezi mitatu kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya cha Bulela kilichopo katika Kata ya Bulela mkoani Geita.
.
Agizo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe.Staslaus Mabula, wakati wa majumuisho ya ziara ya Kamati hiyo, ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Mji wa Geita, mkoani Geita.
.
Mhe.Mabula amesema kituo hicho kitaendelea kutoa huduma huku kikifanyiwa marekebisho mbalimbali ikiwemo kubadilisha sakafu na milango ambayo haina ubora, ambapo pia ameishauri Halmashauri hiyo kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba ili kituo hicho kinapokamilika kiweze kuwa na vifaa vitakavyoweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
.
Pia imependekeza chumba cha upasuaji kikamilishwe kwa wakati na kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa vifaa ili kuanza kutoa huduma za upasuaji kwa mama wajawazito.
.
"Chumba cha upasuaji ni eneo muhimu sana kwa kuwa huko ndipo tunapowalenga wamama wajawazito wenye changamoto kupata matibabu hivyo hakikisheni inakamilika na vifaa vinakuwepo," amesisitiza Mabula.
.
Aidha, Mabula amewataka kuhakikisha wanajibu hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na za kamati ili kuzifuta na kuziondoa kabisa.