
Rais wa Zanzibar na ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi azindua fursa za uchimbaji mafuta na gesi Zanzibar, ambapo amezialika kampuni zote za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kushiriki katika Duru ya kwanza .
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo, alipozindua Duru ya kwanza ya Utoaji wa vitalu kwa Kampuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia maeneo ya baharini Zanzibar, katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip.
Rais Dk.Mwinyi amewakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji , wawekezaji wote wa sekta ya mafuta na gesi .
Aidha Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa dhamira ya Serikali katika uchumi wa buluu, ni kuimarisha uchumi wa nchi kwa haraka, na kuhakikisha upatikanaji wa maendeleo endelevu, ya vyanzo vya nishati ya uhakika.
Kwa upande mwingine Rais Dk.Mwinyi, amesema Serikali inaamini kuwa uchumi wa Buluu una fursa nyingi za kukuza mipango ya maendeleo ya kiuchumi, yenye lengo la kupunguza umasikini na kutengeneza fursa za ajira nchini.
