
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda, ameziagiza Halmashauri zote nchini zilizokopeshwa fedha kwa ajili ya programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi (KKK) kutafuta vyanzo vingine vya fedha kwa ajili ya kuzirejesha ili Halmashauri nyingine zinufaike na mkopo huo.
Mhe.Pinda alitoa kauli hiyo mkoani Shinyanga wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipotembelea na kukagua utekelezaji mradi wa Uimarishaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini (LTIP) katika eneo la Ibadakuli.
Kauli ya Mhe.Pinda inafuatia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kutaka kujua hatua zinazochukuliwa na wizara baada ya kuelezwa kuwa, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ni mojawapo ya halmashauri zilizopewa fedha hizo ambapo ilipata shilingi bilioni 1.055 na kushindwa kuzirejesha kwa mujibu wa makubaliano.
Kwa mujibu wa Mhe. Pinda, wizara yake kwa sasa haiangalii tena malengo ya mradi katika kupata fedha na badala yake inaenda mbali zaidi ili halmashauri zitumie vyanzo vingine kulipa deni na wakati huo halmashauri hizo zikitumia vyanzo vingine kupata fedha.
