
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda, amewataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuacha kuwahudumia wananchi kwa kuangalia hali zao na badala yake watende haki katika kutoa huduma.
Mhe.Pinda ametoa kauli hiyo, wilayani Ruangwa mkoani Lindi wakati wa kufunga Mkutano wa Wadau katika ngazi ya Wilaya kujadili mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi nchini, mkutano uliofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa.





Amewaambia watendaji wa sekta ya ardhi kupitia mkutano wa wadau kuwa, pale wanapopokea mwekezaji sehemu ambayo tayari ina mipango ya matumizi ya ardhi basi taratibu zizingatiwe na kusisitiza pasiwe na suala la kuvamia vijiji vilivyowekewa mipango ya matumizi.
Mbali na suala hilo Mhe. Pinda ameelezea suala la ushirikishwaji wananchi kwenye kupanga mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji ambapo amesema ushirikishwaji wadau ni kipaumbele namba moja kwenye mradi wa uboreshaji miliki za ardhi na ushirikishwaji huo unaanzia ngazi ya kijiji hadi taifa kwa lengo la kuwafanya wananchi kuuelewa mradi ipasavyo.
Akitolea mfano wa wilaya ya Ruangwa, Mhe.Pinda amesema ushirikishwaji katika wilaya hiyo umelenga kupata taarifa ya utekelezaji katika wilaya na baadaye wadau kutoa maoni yao.
Katika mkutano huo wa siku moja wa wadau, mgeni rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Majaliwa alizindua Ripoti ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi ya Vijiji katika wilaya ya Ruangwa na kutoa vyeti 18 vya ardhi ya Vijiji.
Waziri Mkuu amewaeleza washiriki wa mkutano huo wa wadau kuwa, nia ya serikali ya Tanzania ni kupima ardhi yote ili wananchi wakiwemo wana vijiji waweze kuitumia kwa maendeleo ya shughuli za kiuchumi.
Aidha, amewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri nchini kushirikiana na wizara ya ardhi kufanikisha mradi wa uboreshaji milki za ardhi nchini.
Mradi wa Uboreshaji Milki za Ardhi (LTIP) katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa unalenga kuvifikia vijiji vyote kwa lengo la kuvihakikishia vinapata mafanikio.
