
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ali Hapi ameagiza watu wote wanaomiliki viwanja walivyopewa na serikali katika miradi mbali mbali iliyopita ya upimaji hasa katika kata zote za wilaya ya Kinondoni kufanya usafi wa viwanja hivyo kabla taratibu za kisheria hazijawakuta.
Mh. Hapi ameyasema hayo kata ya Mbweni Jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kukagua mashamba na viwanja visivyoendelezwa ambapo amewataka wamiliki wote wa viwanja hivyo ndani ya muda mchache kufanya usafi kabla ya kuanza kuviorodhesha ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao ikiwemo kupeleka maombi kwa Mh. Rais ili wamiliki wafutiwe hati zao kutokana na kushindwa kuviendeleza.
Mapema akiwa katika nyumba ya Bw. Joseph Michael maarufu Mandojo iliyobomolewa kwa kile kilichodaiwa kuwa ni amri ya Mahakama na baadhi ya wamiliki wengine katika eneo hilo pia amewataka wamiliki wote akiwemo msanii huyo aliyebomolewa kufika ofisini kwake na nyaraka zote na viongozi wote kuanzia ngazi za mtaa ili kuangalia uwezekano wa kumaliza mgogoro huo ikiwemo na kuangalia taratibu za ubomoaji kama zilifatwa.