
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt.Binilith Mahenge amesema Serikali ngazi ya mkoa inatafuta suluhu ya kudumu ya mgomo wa Madereva wa Daladala ulioibuka leo ili kufanya shughuli za usafirishaji wa abiria zirejee katika hali yake ya kawaida.
Mapema leo asubuhi Madereva wa magari ya kusafirisha abiria maarufu kama daladala mkoani Dodoma walimefanya mgomo kupinga hatua ya Serikali ngazi ya mkoa kuwahamisha katika vituo walivyovizoea ambavyo vipo katikati ya mji huo.
Madereva hao wamesema wamefikia hatua hiyo kufuatia kupuuzwa kwa maombi yao ya kuwekwa katika kituo ambacho kitakuwa na mazingira rafiki kwao kikazi na abiria wanaowapakia.
Msemo wa waswahili usemao kufakufaana umeonekana leo Dodoma baada ya kutokea mgomo ambapo hali hiyo ilionekana ahueni kwa Madereva wa pikipiki za matairi matatu maarufu kama Bajaji pamoja na Bodaboda wakionekana wakifanya shughuli ambazo zilikuwa zifanywe daladala kwa kuwabeba abiria kwa nauli za juu kulinganisha na zile za kawaida.