Back to top

BIL. 5 KUREJESHA MIUNDOMBINU ILIYOHARIBIKA LINDI

03 May 2024
Share

Serikali imetoa shilingi bilioni 5 ambazo ni fedha za dharura, kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja yaliyoharibika, katika Mkoa wa Lindi, kufuatia mvua kubwa za El-Nino zilizonyesha, na kuleta athari katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo, ameyasema hayo alipotembelea na kukagua hatua za ujenzi zinazoendelea, katika daraja la Somanga linalounganisha Mkoa wa Dar es Salaam - Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma ambalo lilikatika kutokana na mvua.

Zengo amewataka wananchi wanaoishi karibu na barabara, kuacha kufanya shughuli za kibinadamu kwenye kingo za barabara, pamoja na kutupa taka ngumu katika mitaro, kwani kufanya hivyo kunasababisha maji kushindwa kupita pindi mvua zinaponyesha. 

Kwa upande wake Msimamizi Kitengo cha Matengenezo TANROADS, Mkoa wa Lindi Mhandisi Robert Mosea,  ametaja barabara ambazo zimeathiriwa na mvua hizo na zinaendelea na matengenezo ni Kilwa Masoko – Nangurukuru mpaka Liwale, Barabara ya Liwale – Nachingwea, Nachingwea mpaka Kilimarondo pamoja na Barabara ya Tingi – Kipatimo.