Back to top

WANANCHI WAPONGEZA KASI YA UREJESHAJI MIUNDOMBINU MOROGORO.

18 May 2024
Share

Baadhi ya wananchi katika Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, wameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuhakikisha kuwa inarejesha kwa haraka miundombinu ya barabara na madaraja ili iweze kupitika.

Wamesema kuwa uharibifu wa barabara ulisababisha wananchi kutumia usafiri wa pikipiki, ambao walikuwa wanatozwa kati ya shilingi 20,00 mpaka 30,000 kwa umbali usiozidi Kilomita 20 kuelekea Makao Makuu ya wilaya ya Malinyi katika eneo la Mtimbila.

Wamesema kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika mkoa huo zimesababisha maji kupita juu ya barabara na kusababisha mmomonyoko katika kingo za barabara na baadhi ya makalvati na madaraja hivyo kuathiri miundombinu hiyo iliyopelekea shughuli za kiuchumi kusimama kwa muda.

Kwa upande wa madereva wanaofanya usafirishaji wa watu na bidhaa kwa kutumia trekta Haidari Shaban na Mohamed Ramadhan wakazi wa Ifakara wamekiri kuwa usafiri wa trekta unaharibifu barabara huku wakiwasihi madereva wengine kuacha kutumia barabara hizo kipindi hiki cha mvua.


Akizungumza mara baada ya kukagua urejeshaji wa miundombinu, katika barabara ya Lupilo-Malinyi Bw. William Sungura ambaye ni Mhandisi Mwandamizi Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Morogoro, amesema kuwa serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha inarudisha mawasiliano, hususani kwa maeneo yaliyokuwa yamekata mawasiliano.


Aidha ametoa rai kwa madereva wanaotumia trekta kuwakwamua madereva wengine barabarani na kujikwamua wanapokuwa wamekwama kutoacha mashimo mara baada ya kujikwamua kwani jambo hilo linalosababisha barabara kujifunga na kuongeza changamoto zaidi ya uharibifu.