
Leo Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Chai Duniani, ambapo wakulima na wadau wa zao la chai hapa nchini wamelalamikia bei ndogo ya zao hilo, gharama za uzalishaji kuongezeka pamoja na ucheleweshwaji wa malipo kwa wakulima pindi wanapopeleka viwandani.
Wakizungumza wakati wa Maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dodoma, wakulima wamesema changamoto nyinginewanayokutana nayo ni kufungwa kwa baadhi ya viwanda vya chai kwenye baadhi ya mikoa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chai Bw. Mustapha Umande amesema bodi itaendelea kusimamia zao hilo, ili lilete tija kwa wakulima na wanafanya kila jitihada kuondoa changamoto zinazowakabili wakulima wa zao la chai.
Akieleza juhudi za serikali katika kuondoa changamoto za wakulima wa zao cha chai Naibu Waziri wa Kilimo Mh. David Silinde, amesema imeanza kutatua changamoto za wakulima wa chai ikiwemo kuanzisha soko la chai sambamba na kuanza kujenga viwanda vya kuchakata chai ili chai yote ichakatwe hadi hatua za mwisho hapa hapa nchini.
