
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, amesema Bara la Afrika lina nakisi ya bajeti ya miundombinu ya dola za Marekani Bilioni 108 kwa mwaka.
Rais Dokta Samia ameyasema hayo leo aliposhiriki kwenye jukwaa la miundombinu kati ya Korea na Afrika lililofanyika Jijini Seoul Korea Kusini, ambapo amebainisha kuwa, kwa mwaka bajeti ya Miundombinu Afrika ni bilioni 170 wakati zinazopatikana ni bilioni 62 tu.
Pamoja na kwamba miundombinu ndio moyo wa Uchumi, Dokta Samia amesema katika utekelezaji wake Afrika inakabiliwa na changamoto ya vipaumbele vinavyoshindana ikiwemo utoaji wa huduma za jamii na hivyo kufanya bajeti yake kutojitosheleza.
Hata hivyo Rais Samia ameendelea kuikaribisha Korea Kusini pamoja na sekta binafsi kuongeza uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu hasa Reli na Gesi pamoja na miundombinu ya Kidigitali.
Awali akifungua mkutano huo, Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Usafirishaji Sang-Woo Park, amesema kuna uwezekano mkubwa wa kuwekeza Afrika kutokana na kuwa ni bara la pili kwa ukubwa lenye idadi ya watu bilioni 1.3 rasirimali nyingi.
Mkutano huu wa Jukwaa la miundombinu ni sehemu ya Mkutano wa wakuu wan chi za Afrika na Korea wenye lengo la kuimarisha ushirikiano ambao umeanza jana.
