
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bi. Grace Quintine, ameishauri Wizara ya Fedha kuhakikisha Watanzania wote nchini wanapatiwa elimu ya fedha ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha na waweze kufanya maamuzi sahihi katika matumizi sahihi ya vipato vyao.
Bi. Quintine ametoa ushauri huo alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika wilayani Urambo mkoani Tabora, kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi ili waweze kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika Sekta ya Fedha na kujikomboa kiuchumi.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, Bw. Sabhi Makongo, alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali ya masuala ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali ikiwemo watumishi, wanavikundi vya kinamama na Jamii katika ngazi ya familia.
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, alisema wapo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa masuala ya fedha.
Katika zoezi la kutoa elimu kwa Wananchi Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha imeambatana na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) ikiwa ni Utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.
