Back to top

UCHAGUZI USIMAMIWE NA TUME HURU YA UCHAGUZI

16 August 2024
Share

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amesema chama hicho kinataka uchaguzi wa Serikali za Mitaa usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi na sio wanasiasa.

Bi.Dorothy Semu, amebainisha haya siku moja baada ya serikali kutoa tangazo la uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.

Jana 15 Agosti 2024, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe.Mohamed Mchengerwa, alitangaza kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2024, utafanyika Novemba 27, 2024, uchaguzi utakaowachagua Wenyeviti wa Vijiji na Wajumbe wa Halmashauri ya Vijiji, Wenyeviti wa Mitaa na Wajumbe wa Halmashauri ya Mitaa pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji kwa Halmashauri za Wilaya.

Waziri Mchengerwa Pia alimuelekeza Mkurugenzi wa TAMISEMI kuhakikisha kuanzia Agosti 16, 2024 elimu ya upigaji kura inaanza kutolewa kwa wananchi ili waweze kufahamu namna ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Waziri Mchengerwa amelisema fomu za wagombea wa nafasi hizo ambao ni kutoka vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu zitaanza kutolewa Novemba Mosi hadi 07, 2024 na kampeni za uchaguzi zitaanza Novemba 20 hadi 26,2024.

Aidha Mchengerwa alibainisha ukomo kwa viongozi waliopo sasa kuwa ni Oktoba 28, 2024.