
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.Pindi Chana, ameupongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa jitihada zake za kulinda maeneo ya misitu nchini na kuwasisitiza kuwa wabunifu na kuongeza mashamba ya Miti.
Dk.Chana ametoa pongezi hizo wakati wa kikao na Menejimenti, Maafisa na Maaskari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kilichofanyika Makao makuu ya TFS Misitu House Itega jijini Dodoma.
“Hongereni kwa kazi nzuri za ulinzi mzuri wa misitu na uhifadhi, kuna mvua za kutosha, chakula cha kutosha na ninawaahidi ushirikiano wa kutosha na milango yangu iko wazi” amesema Mhe. Chana.
Aidha Dk.Chana ameitaka TFS kuwa mfano bora wa kuigwa, katika masuala ya uhifadhi na utunzaji wa misitu na kutumia Teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao akitolea mfano matumizi ya ndege nyuki “drones”na helikopta.
"Tusikubali misitu ipungue kwa sababu tumepewa dhamana ya kuisimamia, ulinzi wa maeneo tuliyokabidhiwa ni wajibu wetu"amesema Mhe.Chana
