
Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu, amesema chama hicho kimejiandaa sawia kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu.
Semu amebainisha hayo leo, wakati akihutubia katika ufunguzi wa Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya ACT Wazalendo kwenye Ukumbi wa Hichilema, Makao Makuu ya Chama Jijini Dar es Salaam.
" OR- TAMISEMI imetangaza uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka 2024. Chama tumejiandaa vyema kushiriki, na leo itakuwa ajenda kubwa, tutajadiliana namna tunavyopaswa kujiandaa, kujipanga na kuhakikisha uchaguzi huu unatuweka katika nafasi nzuri ya ushindi," Semu.
Amedai kuwa chama Tawala na Serikali yake kimeanza kuonesha hila kuelekea kwenye uchaguzi huo huku akidai kuwa wameanza kubinya uhuru wa vyama na wananchama.
Hata hivyo Semu amesema wameshapeleka kesi mahakamani kuzuia Wizara ya TAMISEMI kusimamia uchaguzi huo.
Kadhalika Semu amesema Watanzania wameanza kuingiwa tena na hofu kwa kukithiri kwa matukio kuogofya nchini.
"Inasikitisha zaidi kuona watu wa kwanza wanaohusishwa na matukio haya ni Jeshi la Polisi na baadhi ya matukio wananchi wanalalamikia Polisi kutochukua hatua za haraka kwa wanaohusika na matukio hayo" Amesema Semu.
