
Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Arusha zimesababisha kifo cha mtu mmoja katika eneo la Majengo huku pia zikiharibu miundombinu, na mali za wananchi hasa wanaoishi kwenye maeneo ya Bondeni na kwenye mikondo ya maji baada ya nyumba zao kujaa maji.
ITV imeshudia Polisi wakiondoa mwili wa mtu huyo kwenye eneo la tukio huku wananchi wa mtaa huo wa majengo wamesema mtu huyo ambaye ni mwanamke na jina lake halijafahamika wamemuona akielea kwenye Mtaro wa maji nje ya nyumba zao.
Viongozi wa eneo hilo wamelalamika kuwa maji yanayoingia kwenye nyumba zao ni matokeo ya ujenzi wa miunodombinu ya barabara na wamewalaumu wakandarasi kwa kuelekeza maji kwenye makazi yao.
Hata hivyo meneja wa wakala wa barabara TANROAD mkoa wa Arusha Bw. John Kalupale pamoja na kukiri kupokea malalamiko ya wananchi kuhusu mitaro ya maji kila mvua zinaponyesha amesema changamoto kubwa ni kuzibwa kwa mikondo ya maji kunakotokana na shughuli za binadamu na kwamba wanaendelea kuzitatua zilizoko ndani ya uwezo wao na zingine zinaendelea kutatuliwa na ngazi za utawala
Bw. Kalupale amesema pia lipo tatizo la wananchi kugeuza mitaro ya maji kama madampo ya kutupa takataka linalochangia mitaro kuziba na maji kupoteza mwelekeo na kuingia kweye nyumba za watu.
Jitihada za kuwapata mkurugenzi wa jiji na mkuu wa wilaya ya Aarusha kuelezea hatua za kiutendaji na kiutawala zinaochukuliwa kukabiliana na changamoto zinalalamikiwa zinaendelea baada ya kudai kuwa wanatembelea maeneo husika na watatoa taarifa baadaye.