Back to top

KAMPENI YA KITAIFA YA AFYA YA AKILI YAENDELEA JIJINI DODOMA

18 May 2025
Share

Hospitali Bingwa ya Taifa ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe imehimiza umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili na kula mlo kamili kama njia ya msingi ya kulinda na kuimarisha afya ya akili.

Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili kutoka hospitali hiyo, Dkt. Enock Chagarawe, kuwa hatua hiyo ni  mwendelezo wa Kampeni ya Kitaifa ya Afya ya Akili inayoendelea jijini Dodoma inayolenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu ustawi wa afya ya akili.

Dkt. Chagarawe, amesema afya ya akili ni hali ya kuwa na utimamu wa kiakili na uwezo wa kushirikiana na watu wengine bila kujitenga. 

Amebainisha kuwa matatizo ya afya ya akili huanza kwa mtu kuwa na msongo wa mawazo, hali ya kuwa na mawazo mazito au hofu bila kuwa na dalili za wazi za ugonjwa wa akili.

"Dalili nyingine ni pamoja na mtu kuamini kwamba amerogwa au kwamba watu wanamnyemelea kwa nia mbaya, kusikia sauti ambazo hazipo, kujitenga, kujiona hana thamani na hata kutamani kifo na wengne kuonesha tabia za hasira za mara kwa mara na kuwa wagomvi," ameeleza Dkt  Chagarawe.

Amefafanua kuwa watu wenye ugonjwa wa akili wanapaswa kupata matibabu ya kitaalam katika hospitali na wakati mwingine kulazwa kwa ajili ya uchunguzi na tiba sahihi sambamba na huduma ya ushauri nasaha kutoka kwa wataalam wa saikolojia pia ni muhimu katika mchakato wa matibabu.

Kampeni ya kitaifa ilianza mkoani Dodoma, na tayari imeshatembelea mikoa ya Singida na Iringa, huku mikoa ya Morogoro na Manyara ikiwa katika ratiba inayofuata. Kaulimbiu ya kampeni inasema, "Afya ya Akili ni Afya – Jikubali, Jijali."

Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kubadili mtazamo wa jamii kuhusu afya ya akili na kuhamasisha watu kutafuta msaada mapema.