
Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa miradi yote ya umwagiliaji inakamilika kwa wakati na inaleta tija kwa wakulima nchini.
Ameeleza haya wakati wa ziara yake ya kikazi katika mradi wa umwagiliaji uliopo wilayani Masasi, mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kukagua taasisi zilizo chini ya Wizara ya Kilimo.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa bwawa pamoja na uchimbaji wa mifereji ya umwagiliaji, ambao ukikamilika unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wakulima 700 kutoka Vijiji saba, ambapo Waziri Chongolo amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa bwawa hilo litachochea uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga, mpunga na mahindi na kusisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inapaswa kusimamia kwa umakini utekelezaji wa miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na wakulima wanapata uzalishaji wenye viwango bora.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amesema Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya umwagiliaji ili wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara wanufaike na kilimo cha umwagiliaji, hatua itakayowawezesha kulima bila kutegemea mvua.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Tellack, amewataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu ya miradi ya umwagiliaji ili idumu kwa muda mrefu.
