Back to top

ZANZIBAR SASA YAPOKEA WATALII LAKI 1 KILA MWEZI

10 February 2026
Share

Baada ya kuapishwa kwa Mhe. Rais  Dkt. Hussein Mwinyi kuongoza Zanzibar katika awamu ya nane ya uongozi, sekta ya utalii imeonesha ukuaji mkubwa na wa kasi. 

Katika mwezi wa kwanza wa uongozi huo, idadi ya watalii ilikuwa takribani 72,000 pekee.

Hata hivyo, kwa sasa kuanzia Novemba hadi Januari, Zanzibar imepokea wastani wa watalii laki 1 kwa kila mwezi.

Ukuaji huu unaunganishwa na takwimu za jumla zinazoonesha kuwa Zanzibar imefanikiwa kupokea zaidi ya watalii milioni 1, jambo linalothibitisha wazi kuwa soko la utalii linaendelea kukua kwa kasi na masoko mapya ya Kimataifa yanafunguka kwa nguvu kubwa.

Kwa sasa, Zanzibar inapokea watalii kutoka masoko makubwa ya Kimataifa ikiwemo Italia, Ujerumani, Ufaransa, Marekani, Poland pamoja na nchi za Skandinavia. 

Aidha, kuna ukuaji mkubwa wa soko la Poland, ambalo linaonesha kasi ya kipekee.

Masoko mengine yanayochipukia kwa nguvu ni China, India na Ukraine, yakiongeza wigo wa watalii wanaoitembelea Zanzibar.

Ni muhimu kukumbuka kuwa wakati Dkt. Hussein Mwinyi anaingia kwenye awamu yake ya kwanza ya uongozi, dunia ilikuwa katika kipindi kigumu cha janga la UVIKO-19, ambapo Sekta ya Utalii Zanzibar ilishuka kwa kiwango cha asilimia  -51%. 

Kupitia mikakati madhubuti, ufunguzi wa masoko na diplomasia ya kiuchumi, sekta hii imefanikiwa kurejea na kukua hadi kufikia asilimia 24 katika awamu ya pili, na sasa inaendelea kukua kwa kasi ya takribani asilimia 25.

Leo hii, idadi kubwa ya watu wanaoitembelea Zanzibar si tu wanakwenda kwa mapumziko, bali pia wanakuwa mabalozi wa utalii kwa vitendo kwa kuhamasisha na kuwaleta wenzao, pamoja na kuitangaza Zanzibar Kimataifa kama kivutio salama, chenye amani na fursa nyingi.