Back to top

"LISSU ALISEMA HAKUTAKUWA NA UCHAGUZI" MASHAHIDI

16 February 2026
Share

Mashahidi wa kificho wawili wa upande wa Jamhuri ambao wamejitambulisha kama wafuasi wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), wametoa ushahidi wao katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam dhidi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu ambaye anashtakiwa kwa mashtaka ya kosa la uhaini.

Mashahidi hao ni wa saba aliyepewa jina la siri kama (P2) ambaye ni fundi umeme, mkazi wa Songea mkoani Ruvuma ni shahidi wa nane ni (P8) ambaye ni Mfanyabiashara wa matunda soko la Manyema, akiwa mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Wawili hao waliongozwa na wakili Mkuu wa Serikali, Ignas Mwinuka na Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga, ambapo wametoa ushahidi wao kwa nyakati tofauti mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru.

Shahidi huyo wa saba ambaye ni mfuasi wa CHADEMA tangu 2021, amedai kuwa alimuona Bwana Lissu akiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari akitoa maelezo kwamba hakutakuwa na uchaguzi wa Oktoba 2025 na wanaotaka kugombea Ubunge na Udiwani wasahau.

Shahidi huyo aliyekuwa ndani ya chumba maalum alidai kuwa Lissu alisisitiza namna ya kuzuia uchaguzi mkuu usifanyike ili kuleta mabadiliko, akihamasisha kila mmoja awe jasiri.

Alipoulizwa na wakili Mwinuka nini kiliendelea amedai kuwa alimfuata kiongozi wake wa Baraza la Vijana na baada ya kufanya mawasiliano Aprili 7, 2025, waliambiwa mkutano utafanyika Ruvuma Aprili 10, 2025 na watoa mchango kwa njia ya tone tone.

Aidha shahidi huyo amedai kuwa ilipofika Aprili 9, 2025 akiwa katika shughuli zake alifuatilia pia taarifa za habari aliona kwamba Tundu Lissu, amekamatwa na licha ya Lissu kukamatwa, ilipofika Aprili 10, 2025 alijiandaa na kwenda kwenye mkutano huo uliofanyika Ruvuma ambapo alikuta magari ya Polisi ambao walisema hakutakuwa na mkutano.

Amedai kuwa baada ya hapo alitoka eneo la mkutano na kuelekea ofisi za chama baada ya kusikia Makamu Mwenyekiti atakuwa eneo hilo na alipofika alikutana na viongozi wengine pamoja na waandishi wa habari na kabla mkutano haujaanza yalifika magari ya Polisi na wakaambiwa wapo chini ya ulinzi kisha wakakamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi kilichopo karibu na ofisi za mkuu wa mkoa.

Akihojiwa na Wakili Katuga shahidi wa nane amesema yeye ni mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro anajishughulisha na biashara ya matunda katika Soko la Manyema, Mbuyuni.

Shahidi huyo wa nane amesema aliingia kwenye akaunti ya Jambo TV, ambapo aliona na kusikia tamko la mshtakiwa Tundu Lissu, akisema lazima tufanye uhasi dhidi ya serikali na tutakinukisha, pia alisema tutaenda kuzuia uchaguzi unaokuja kama hakuna mabadiliko.

Akiendelea kutoa ushahidi wake amesema aliipata hamasa kuwahamasisha vijana wenzake hasa kupitia kauli ya No Reform/ No Election na akaanza kuwaonesha vijana wenzake zile video za mshtakiwa Bwana Tundu Lissu akiwa anahutubia na walikuwa wanasubiri kauli ya Mheshimiwa wakakinukishe, wafanye uasi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 17 kwa ajli ya kuendelea na Ushahidi.

Katika kesi hiyo Bwana Tundu Lissu, anashtakiwa kwa kosa moja la Uhaini kinyume na kifungu cha 39 (2) cha sheria ya kanuni ya adhabu ambapo inadaiwa mnamo Aprili 3,2025 maeneo ya Kinondoni mkoa wa Dar es Salaam akiwa chini ya utii na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitamka maneno yenye nia ya kuzuia uchaguzi wa 2025.