Back to top

MAKAMU WA RAIS AONGOZA MIAKA 120 YA MASHUJAA WA VITA YA MAJIMAJI

27 February 2026
Share

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Mashujaa wa Vita ya Majimaji wanapaswa kuenziwa kwa kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi, kupinga masuala ya ukabila na kutambua wajibu wa pekee wa kulitetea na kulipigania Taifa.
 
Makamu wa Rais amesema hayo, wakati wa kilele cha Tamasha la 17 la Kumbukizi ya Miaka 120 ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji, lililofanyika katika Viwanja vya Makumbusho ya Vita ya Majimaji, Songea mkoani Ruvuma. Amesema ni muhimu kuwaenzi mashujaa hao kwa kuendelea kusimamia umoja ili kuhakikisha makabila yote yanakuwa Taifa moja, kufanya kazi kwa bidii kuijenga Nchi, pamoja na kupinga vitendo vya rushwa na kutenda haki.
 
Ameongeza kwamba, Mashujaa wa Vita ya Majimaji waliweka pembeni ubinafsi kwa kuunganisha makabila zaidi ya 30 ili kuweza kupambana na wakoloni na hivyo kutengeneza mustkabali mzuri wa maisha ya sasa.
 
Makamu wa Rais, amesema kumbukizi ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji ni muhimu katika kuwezesha kizazi cha sasa na kijacho, kuona na kujifunza jinsi ambavyo mashujaa hao walivyojitolea maisha yao katika kulinda heshima, utu na rasilimali za Taifa.
 
Aidha, Makamu wa Rais ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Shirika la Makumbusho ya Taifa kuanzisha Makumbusho katika maeneo yao ili kuendelea kuhifadhi historia nzuri ya Taifa, pamoja na kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye Malikale zilizopo nchini ikiwemo kuinua uchumi kupitia utalii wa utamaduni.
 
Amesema maboresho makubwa yaliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika Sheria ya Malikale, Sura 333 na Sheria ya Makumbusho ya Taifa, Sura 281, yametoa fursa kwa jamii kuanzisha Makumbusho.
 
Pia, ametoa wito kwa Taasisi binafsi na jamii kwa ujumla, kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuwekeza na kutumia kumbukumbu zilizopo nchini, kama chanzo cha ajira na majukwaa ya kutangaza bidhaa na vivutio vya uwekezaji na utalii.
 
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya Songea – Makambako na inatarajia kuanza ujenzi wa awamu ya kwanza barabara hiyo hivi karibuni kwa kuwa tayari mkandarasi amepatikana.
 
Awali, Makamu wa Rais alishiriki tukio la uwekaji wa silaha za jadi katika mnara wa kumbukumbu ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji pamoja na kuweka shada la maua katika makaburi waliozikwa mashujaa hao.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Makambusho ya Taifa Dkt. Noel Lwoga, amesema pamoja na kufanya kumbukizi ya kuwaenzi Mashujaa wa Vita ya Majimaji, lakini pia malengo mengine ni kurithisha urithi wa historia , mila na desturi kwa kizazi cha sasa na baadaye, kuibua na kuendeleza fursa za utalii na uchumi zinazotokana na historia na utamaduni pamoja na kuelimisha umma wa Watanzania umuhimu wa kutunza na kuhifadhi urithi wa Taifa.


Makumbusho ya Vita vya Majimaji  yalianzishwa mwaka 1980 chini ya Ofisi ya Mkoa wa Ruvuma na Baraza la  Makumbusho ya Majimaji, Mila na Desturi, na baadaye kupandishwa hadhi na kuwa Makumbusho ya Taifa ya Vita vya Majimaji mwaka 2009.
 
Tamasha la 17 la Kumbukizi ya Miaka 120 ya Vita vya Majimaji limebeba kaulimbiu isemayo “Utamaduni wetu ndiyo nguvu yetu kwa maendeleo ya utalii na uchumi”  ambapo limewashirikisha Viongozi, Wananchi, wadau mbalimbali wa utalii na utamaduni na Viongozi wa Kimila kutoka Tanzania, Zambia, Msumbiji, Malawi, na Afrika Kusini.