Back to top

EPUKENI CHOYO NA WIVU KAZINI- MHE.CHANDE

17 March 2026
Share

Watumishi umma wametakiwa kuwa wabunifu, kutafiti na kuzingatia utu, uaminifu na uadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza tija kwa wananchi wanaowahudumia na Taifa kwa ujumla. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) wakati akifungua Baraza la 34 la Wafanyakazi la Wizara hiyo huku linalofanyika Mkoani Lindi na kuwataka watumishi hao kutumia muda mwingi kutafuti na kubuni mazao mapya ya utalii yatakayosaidia ongezeko la siku za watalii kukaa nchini na kuongeza pato la Taifa. 

Amewataka watumishi hao kuwa wavumilivu, wastahimilivu na wasiri katika utendaji wa kazi, sambamba na kujifunza na kujiendeleza na kuwataka kujiepusha na wivu, choyo na husda katika  utendaji. 

"Niwaombe sana kuendelea kushirikiana kama ambavyo mnashirikiana, kujiepusha na choyo, wivu na husda katika maeneo yenu ya kazi, kumtanguliza Mungu mbele, kuthaminiana, kutoa fursa za masomo za kujiendeleza kwa wafanyakazi na motisha ili kuwa chachu kwa wengine kufanya kazi vizuri” Amesisitiza Mhe. Chande.

Aidha, Mhe. Chande amesisitiza juu ya kuongeza nguvu katika kulinda Wanyamapori waliopo kukuza idadi ya watalii kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan idadi ya watalii Ml. 8 ifikapo 2030 kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo kuongeza tafiti na ubunifu na kuweka mikakati ya makusudi ya kuibua  vivutio vipya vya utalii.


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Nkoba Mabula, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara amesema kupitia Baraza hilo wajumbe watapata fursa ya kujua mpango wa bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 na makisio ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027. 

“Wajumbe kupitia mkutano huu, watapata elimu juu ya mango mkakati wa kupambana na rushwa, huduma za mfuko wa fidia kwa wafanyakazi na sera ya huduma ya taifa kwa wote pamoja na mabadiliko ya huduma kutoka kwa wataalamu wa mfuko wa bima ya Taifa” amesema Nkoba.

Naye, Mwakilishi wa Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Bw. Samwel S. Nyungwa Katibu TUGHE Dodoma amesisitiza wajumbe hao kuzingatia haki na wajibu wa utumishi wa umma sambamba na kutekeleza majukumu kwa kiwango cha juu wakati wa ajira na baada ya kustaafu.